Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, tulifanya mahojiano na Yusuf Tazegun, mmoja wa wanazuoni wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Ahlul-Bayt wa Uturuki (EHLADER), kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu. Yeye ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa Hawza ya Qom, pamoja na kuwa mtafiti na mwandishi, alisema kuwa; katika kipindi chake cha usomaji alipata athari kubwa zaidi kutoka kwa Imam Khomeini (r.a), Allama Tabatabai (r.a) na Allama Misbah Yazdi (r.a). Yafuatayo ni maudhui kamili ya mahojiano hayo:
Swali: Kwanza tunakushukuru kwa kukubali mwaliko wetu. Kama unavyofahamu, tupo katika siku za maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 yana maana gani kwako? Je, unayaona kama mabadiliko ya kisiasa tu au kama harakati ya ustaarabu kwa maana pana zaidi?
Yusuf Tazegun: Kuyafasiri Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 kama mabadiliko ya uongozi tu ni kutotambua roho yake halisi. Bila shaka, kulikuwa na mabadiliko ya mfumo na mpito kutoka utawala wa kifalme kwenda Jamhuri ya Kiislamu; lakini mageuzi makuu hayakuwa katika mfumo wa kisiasa, bali katika kiwango cha fikra na itikadi. Mapinduzi hayo yalikuwa ni kujitokeza upya mbele ya madai ya dunia ya kisasa kwamba “dini ni jambo la faragha na binafsi.”
Ninayatazama Mapinduzi kama kurejea Uislamu katika uwanja wa historia katika zama za kisasa kama mhusika hai. Harakati hii ilikuwa jitihada ya kivitendo kuonesha kwamba Uislamu si mkusanyiko wa mafundisho ya ibada na ya mtu binafsi tu, bali una uwezo wa kupanga sheria, siasa, uchumi na utaratibu wa kijamii.
Ustaarabu si miji na taasisi pekee; bali unahusisha taswira ya mwanadamu, mtazamo wa maarifa, uhusiano wa nguvu na maadili, na ufahamu wa uadilifu. Mapinduzi ya Kiislamu yaliingilia moja kwa moja katika maeneo haya na kujaribu kutoa majibu yanayotegemea wahyi kwenye maswali kama: “Ni mwanadamu wa aina gani?”, “Ni jamii ipi?”, na “Ni dola gani?” Kwa mtazamo huu, Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa zaidi ya mapinduzi ya kisiasa; yalikuwa jitihada ya kuelekea uundaji wa ustaarabu.
Swali: Kwa maoni yako, ujumbe mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni upi?
Yusuf Tazegun: Ujumbe mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kanuni kwamba “uhuru na heshima hupatikana tu chini ya kumtii Mwenyezi Mungu.” Mapinduzi yalichukua msimamo dhidi ya udikteta wa ndani na dhidi ya ubeberu wa nje. Kauli mbiu ya “si Mashariki wala Magharibi” haikuwa chaguo la kisiasa tu, bali ilikuwa tangazo la uhuru unaojengwa juu ya kukubali uja wa Mwenyezi Mungu.
Mapinduzi yaliimarisha fahamu miongoni mwa Waislamu kwamba hawalazimiki kufuata itikadi zilizozalishwa na wengine, bali wanaweza kutoa nadharia ya kisiasa na kijamii kwa misingi ya rasilimali na turathi zao za kiakili. Kujiamini huku kulikuwa na umuhimu mkubwa, kwani katika karne ya ishirini jamii nyingi za Kiislamu zililazimika kujitambulisha chini ya kivuli cha ubepari au ujamaa. Mapinduzi ya Kiislamu yalitangaza: “Sisi pia tuna kauli.”
Aliongeza kuwa; Mapinduzi yalizirudisha katika uwanja wa fahamu za kijamii dhana kama kujitoa muhanga, shahada, subira na mapambano ya kusimama imara. Dhana hizi hazikuwa kauli mbiu za kiitikadi tu, bali zilipata uhalisia wa kivitendo katika miaka ya vita na vipindi vya vikwazo.
Swali: Kwa maoni yako, ni sifa ipi iliyo wazi zaidi katika fikra za Imam Khomeini (r.a) kwa Waislamu wa leo?
Yusuf Tazegun: Sifa muhimu zaidi ya Imam Khomeini ni kwamba aliizingatia dini si kwa ajili ya Akhera pekee, bali pia kwa ajili ya kupanga maisha ya dunia. Aliunganisha irfani na siasa, na akaichukulia fiqhi si kama mkusanyiko mkavu wa kanuni, bali kama mfumo hai na mpana unaojumuisha nyanja zote za maisha. Nadharia ya “Wilayat al-Faqih” katika muktadha huu si modeli ya kisiasa tu, bali ni mfumo wa kinadharia wa uongozi wa kijamii wa dini.
Aliongeza kuwa: Katika fikra za Imam Khomeini hakuna mpasuko kati ya siasa na iman. Pamoja na kuwa kiongozi wa kisiasa, alikuwa pia a'rif mashuhuri. Katika vitabu vyake kama “Arubaini Hadithi” na “Adab as-Salah”, alizungumzia utakaso wa nafsi, ikhlasi na safari ya ndani ya mwanadamu. Hivyo, siasa katika mtazamo wake si uwanja wa mashindano ya madaraka tu, bali ni eneo la wajibu wa kimaadili.
Tazegun alisisitiza kuwa; ujumbe mkubwa zaidi wa fikra za Imam kwa Waislamu wa leo ni kuvuka “kizuizi cha hofu.” Imam Khomeini, licha ya mizania ya nguvu za kimataifa, alilijibu swali hili kwa ithbati: “Je, siasa inayojengwa juu ya ukweli inawezekana?” Kuvuka kizuizi hiki cha kisaikolojia ni muhimu sana, kwani tatizo la jamii nyingi za Kiislamu si upungufu wa rasilimali, bali ni ukosefu wa kujiamini.
Swali: Ukiwa miongoni mwa wanazuoni waliosoma nchini Iran, katika kipindi chako cha masomo uliathiriwa zaidi na nani?
Yusuf Tazegun: Katika kipindi changu cha masomo nchini Iran, kilichoniacha athari kubwa zaidi ni nidhamu ya kina ya kielimu ya masomo ya Hawza. Hususan elimu ya Usul al-Fiqhi humzoesha mtu mtazamo wa kimfumo na usio wa juujuu katika kukabiliana na masuala. Mbinu hii haifai tu katika masuala ya fiqhi na dini, bali pia huathiri uundaji wa mfumo mzima wa fikra.
Kwa upande wa haiba, bila shaka sura mbili kubwa ziliacha athari pana — si kwangu tu bali kwa wanafunzi wengi: kwanza Imam Khomeini (r.a) aliyebadilisha mtazamo wetu kuhusu maisha, dunia, dini na siasa; na pili Allama Tabatabai (r.a) aliyekuwa miongoni mwa watu wenye athari kubwa katika uelewa sahihi na wa kina wa dini.
Tazegun pia, akimtaja marehemu Ayatullah Allama Misbah Yazdi, alisema: Namna alivyokabiliana na mikondo ya fikra za kisasa ilikuwa ya kufundisha sana; kwani pamoja na kutetea turathi, hakuyapuuza maswali ya zama mpya.
Mwisho, alisisitiza kuwa: Wakubwa hawa walituonesha kwamba; fikra za Kiislamu si turathi iliyoganda, bali ni mila hai, yenye kuzaa, yenye uchambuzi na yenye uwezo wa kuzungumza na zama.
Swali: Kwa mnasaba wa maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu, una ujumbe gani hasa kwa vijana?
Yusuf Tazegun: Ninachoweza kusema ni kwamba mapinduzi huanzia katika akili na moyo. Ikiwa kijana hatafahamu vizuri vyanzo vyake vya kiitikadi, bila kujua atafikiri kwa dhana za wengine. Leo mitandao ya kijamii, mazingira ya vyuo vikuu na utamaduni wa umma, kila kimoja kinaunda ulimwengu wa maana. Vijana — na kwa hakika sisi sote — tunapaswa kufahamu elimu za kitamaduni na pia kujifunza lugha ya zama. Uwepo wenye athari haupatikani kwa kauli mbiu tu, bali kwa elimu na maadili.
Mwisho, alilishukuru Shirika la Habari la Hawza kwa kutoa fursa ya mahojiano haya na akasema: Tunafuatilia kwa makini maudhui ya kielimu na kifikra ya shirika hili, kwa kuwa yako katika mwelekeo wa kuhuisha mwamko wa Umma wa Kiislamu. Tunaamini kuwa habari, makala na uchambuzi wa chombo hiki vina nafasi muhimu katika uundaji wa mwamko katika ulimwengu wa Kiislamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azibariki na kuzidumisha huduma zenu, na awalipe kwa ubora zaidi wanaofanya kazi katika uwanja huu.
Maoni yako